Mojawapo ya skendo zilizotamba kwenye magazeti
Vichwa vya habari kwenye magazeti vilivyojaa skendo chafu za wasanii wa filamu wa Tanzania
SEKTA ya filamu katika nchi yoyote ile ni sekta yenye nguvu sana, ikizingatiwa kuwa ina uwezo wa kuchangia kwa kiasi kikubwa mno katika uchumi wowote. Sekta hii ina uwezo mkubwa sana wa kuwa kichocheo cha ukuaji wa maendeleo ya haraka na ya kweli ya taifa ya nchi yoyote kwa kuzingatia utamaduni na saikolojia kwa maendeleo halisi na endelevu.
Ingawa sekta ya filamu ni moja tu kati ya sekta nyingi ndani ya tasnia ya burudani inayosimamia ubunifu, lakini filamu zinaaminika kuwa zina uwezo mkubwa sana wa kushawishi ama kutumika kwa ajili ya kuelimisha au kupotosha mambo katika jamii yoyote.
Tasnia ya burudani na ubunifu inajumuisha sekta mbalimbali ikiwemo sekta ya filamu na maigizo, muziki, ulimbwende, mavazi na sanaa zingine za kiufundi, hata hivyo sekta ya filamu ni aina ya sekta inayojipambanua katika kusimamia juhudi za kitaaluma kuhusu uzalishaji na uuzaji wa mawazo katika aina mahsusi ya picha halisi itumikayo kuunganisha mahitaji, matumaini na matarajio ya jamii.
Sinema zinakusudiwa katika kuwapa watu fursa ya kusimulia hadithi zao, na kuwaacha na uhuru wa mawazo kutokana na kuingiliwa na mambo ya kigeni. Kwa hali hii watayarishaji na wasanii wa sinema wa Kitanzania wanapaswa kuishi katika maadili yasiyokinzana na maisha ya jamii na utamaduni.
Kila nikiangalia kwa makini hali halisi ya sekta ya filamu hapa nchini, sioni kama kutakuwa na 'future' yoyote katika tasnia hii endapo mambo yataendelea kuachwa yaende ovyo ovyo kama ilivyo sasa. Ikumbukwe kuwa sekta ya filamu ya Tanzania ni sawa na kinda la ndege linalotegemea mzazi alilishe chakula. Ni kama mtoto anayeanza kutembea, ambaye kila aina ya dosari ni mambo ya kawaida yanayotarajiwa kutokea.
Hata hivyo, katika mazingira ya upatikanaji wa miundombinu ya kimasoko katika kulikuza soko la filamu nchini na kimataifa, Wasanii wa Kitanzania wanastahili kuwa na sifa nzuri katika kuhakikisha kuwa tasnia hii inaaminiwa na watu wote wakiwemo wawekezaji.
Nikiwa mwanaharakati na mdau muhimu sana katika sekta hii, kwa muda mrefu sasa nimekuwa nikijionea vituko hivi na vile kutoka kwa wasanii wetu hasa wanaojiita mastaa, ambao wamediriki kusema kuwa huwezi kuwa maarufu kama huna skendo. Jambo hili linawafanya wasanii wengi katika tasnia hii wasiopenda kujihusisha na kashfa yoyote kukabiliwa na changamoto nyingi za kila siku.
Baadhi ya matatizo haya ni ya asili ya kimataifa, wakati mengine ni ya kipekee kwa jamii mbalimbali.
Miongoni mwa mambo ambayo yamezoeleka sana katika jamii yetu hivi sasa kiasi cha kuzifanya akili zetu kuamini kuwa ni mambo ya kawaida kwa msanii yeyote mwenye umaarufu ni pamoja na kusoma habari zenye kuhusiana na skendo mbalimbali za wasanii wetu. Wasomaji wa magazeti pendwa ambayo wengine hupenda kuyaita ya udaku watakuwa ni mashahidi wa jambo hili, kwani ukifuatilia kwenye magazeti hayo wiki nzima utabaini hili kwa urahisi sana.
Hali hii mara kwa mara imekuwa ikizua malalamiko kwa baadhi ya wasanii wenyewe ambao wamekuwa wakiandikwa kwa mabaya yao wanayoyatenda, na pia hata jamii ambayo imekuwa ikiwafuatilia na kufuatilia habari zao pia. Jambo hili ukilitazama kijuujuu unaweza kuyalaumu magazeti hayo na waandishi wanaowaandika vibaya wasanii kwa kudhani kuwa wanavuka mipaka na kuingilia mambo binafsi, lakini kumbe kuna jambo nyuma ya pazia.
Wasanii karibu wote wa nchi hii, maarufu na hata wasiokuwa maarufu nawafahamu vizuri sana, nimewahi kufanya nao kazi na wengine nimewasaidia kuingia kwenye fani hii ya sanaa ya filamu na maigizo. Ukweli ni kwamba walio wengi huwa wanajipeleka wenyewe kwa waandishi ili waandikwe vibaya kwa dhumuni la 'kutoka kisanii', ndiyo maana wengi wao hata wakiandikwa vipi huwasikii kulalamika au kuchukua hatua zozote. Si hivyo tu, hata pale wasanii hawa wanapohisi kuwa umaarufu wao umeanza kuchuja huwatafuta waandishi wa magazeti hayo ili kuosha nyota!
Wengi wa wanaojiita mastaa wa Bongo waliopata umaarufu kupitia skendo za magazetini huwa hawaijui thamani ya ustaa wao hata pale wanapokuwa tayari maarufu. Hii ni kutokana na skendo zao za ngono mfululizo tunazozisoma magazetini ambazo kwa kweli ni ujinga mtupu!
Inashangaza kuona mtu akitokea kwenye filamu moja au mbili tu, tena kwa kushirikishwa kwenye sehemu ndogo ya sinema hiyo, ataanza kujiita staa na kujiingiza kwenye kujitafutia skendo kwenye magazeti ili asomwe. Ndiyo maana utakuta kila kukicha kunaibuka skendo za aibu kibao!
Mfano ni binti mmoja mwenye asili kama Mmanga ambaye kwa sasa anavuma sana kwa skendo za usagaji kwenye magazeti, ni mwaka jana tu alikuwa akinipigia magoti nimuunganishe aweze kuigiza filamu na wasanii maarufu, siku moja akabahatika kushirikishwa kwenye filamu na mmoja wa wasanii maarufu hapa nchini kwa kupewa sehemu ndogo tu ya kuigiza, eti hivi sasa naye anatembea mabega juu huku akitamba kwenye magazeti kwa kashfa za usagaji, kufumwa na midume usiku na nyingine kibao!
Pia kuna wakati niliwahi kufuatwa na msanii mmoja wa kike (jina nalihifadhi) ambaye wakati huo hakuwa na umaarufu kama alionao sasa, aliyetaka iandikwe skendo yake ya kugombewa na mabwana wawili ambao walikuwa viongozi ndani ya kundi la filamu alilokuwa akifanyia mazoezi. Nilimwelekeza mahali pa kupeleka habari zake huku nikimwambia ukweli kuwa mimi si mwandishi wa kufanya promosheni za aina hiyo, bali mimi ni mchambuzi ambaye naitazama sekta nzima ya filamu, mazuri na changamoto zake na kuihabarisha jamii pasipo kujishughulisha na mambo binafsi ya mtu.
Mifano hai ya wasanii wanaoamini kuwa huwezi kuwa maarufu bila kuibua kashfa iko mingi kiasi kwamba nikianza kuwataja nitajaza kurasa zote za gazeti hili na nisiimalize, japo siyo wasanii wote wanaopenda kuandikwa vibaya kwenye magazeti. Wapo baadhi ya wasanii waliokuwa maarufu sana wakati fulani lakini hawakuwahi kuandikwa vibaya kwenye magazeti, na hawakuwahi kuwafuata waandishi ili wawaandike hata kwa jambo zuri kwani waliamini kuwa kazi zao ndizo zilizokuwa zikiwafanya wajulikane.
Sikatai, wapo baadhi ya wasanii hasa wale wanaolalamika baada ya kuandikwa vibaya kwenye magazeti huwa hawapendi kufuatiliwa katika masuala yao binafsi na kuyaweka kwenye vyombo vya habari, lakini mambo ya kuibuka skendo mbaya kila kukicha yanawafanya hata wasanii wenye maadili mema kuogopa kujitambulisha kwa watu kuwa ni wasanii.
Najua kuwa suala la mapenzi halina mipaka na lingeweza kutokea wakati wowote na kwa mtu yeyote hata kwangu mimi ninayeandika, na kama linatokea kwa wasanii wawili watatu hakuna ubaya wowote, lakini hali ilivyo sasa imekithiri kiasi cha kutia kinyaa.
Utakuta msanii wa kike anajilengesha kwa 'pedeshee' fulani halafu akikubaliwa anamfuata mwandishi wa habari na kumwambia aibue skendo kuhusu uhusiano wake na mtu huyo, tena atamtafutia hata picha. Akishaandikwa gazetini atajifanya kulalamika kuwa waandishi wanamfuatilia maisha yake kwa kuwa yeye ni staa!
Iliwahi kutokea kwa msanii mmoja wa kike aliyetamba sana kwenye magazeti enzi hizo kwa kashfa mbalimbali na baadaye akaingia kwenye ugomvi na aliyekuwa mpenzi wake ambaye ni mwanamuziki maarufu wa bongofleva aliyeamua kumuimba vibaya. Msanii huyu wa kike aliyependa sana kuandikwa vibaya lakini baada ya kuamini kuwa ameshapata ustaa alioutaka hakutaka tena kuandikwa kwa mabaya aliyoyafanya, kiasi cha kujisingizia kunywa sumu.
Pia utakuta msanii wa kiume anaamua kutembeza urijali wake kwa wacheza filamu wa kike karibia wote katika kundi lake akiwa hajali kuwa ipo siku watakuja kujuana, halafu anamfuata mwandishi ili aandike tena ikibidi kwenye ukurasa wa mbele wa gazeti kuwa yeye ni kiwembe!
Ule msemo kuwa “ustaa hauji bila skendo” hauna ukweli wowote, ukijiuliza sana wakati wasanii kama Bishanga, Rich Richie, Waridi, Aisha na wengineo wanavuma walitumia skendo zipi kuwafikisha hapo walipokuwa? Au wasanii kama Lumole Matovolwa (Biggie Poppa), Yusuf Mlela, Kemmi, Monalisa, Natasha na baadhi ya wasanii wa aina yao mbona wamepata umaarufu mkubwa bila kuwa na skendo?
Leo hii imekuwa ni jambo gumu sana kwa wasanii walio wengi endapo utaamua kumwita msanii ukataka kumuandika kwa mazuri yake, kwa kuwa walio wengi wanaamini kuwa mambo mazuri hayawezi kuwafanya watoke.