Search This Blog

Tuesday, June 28, 2011

WASANII NA WACHEZAJI WA BONGO SHULE MUHIMU

KADIRI siku zinavyozidi kwenda na teknolojia pia inakua; hii inahitaji watu pia kuyamudu mazingira haya ya sayansi na teknolojia.
Nchi zinazoendelea hapa duniani huenda sambamba na kukua kwa sayansi na teknolojia ambayo ndiyo inayofanya dunia kuwa kijiji.
Kukua huku kwa sayansi na teknolojia hapa Tanzania kumeleta mambo hasi na chanya kwa wananchi ambapo kwa watu wenye uelewa finyu huyafanya mambo kuwa hasi.
Katika mtazamo wangu wa leo ningependa kuzungumzia wachezaji wa mpira wa miguu na wasanii wa fani mbalimbali ambao wamekwishapata majina lakini sasa shule wameamua kuipa kisogo kwa maana ya kujiendeleza kitaaluma na kujikita zaidi katika kucheza mpira na kuigiza.
Pengine nianzie na baadhi ya wachezaji wa soka ambao wameshapata majina kupitia timu mbalimbali za Ligi Kuu ambao wanakipiga wakiwa wametwaliwa katika shule za michezo (sports academies) ambazo zilikuwa zikiwapa elimu ya soka na taaluma nyingine kwa lengo la kuwa na fani nyingi ili kukabiliana na tatizo la ajira nchini.
Hoja yangu ni kuwa wachezaji hao baada ya kupata majina wamejisahau kujiendeleza kielimu na badala yake wamekalia kucheza soka lakini wakisahau mpira una kupanda na kushuka jambo linaloweza kuwagharimu baadaye kama ilivyowahi kutokea kwa baadhi ya wachezaji.
Nayasema haya nikiwa nimeshuhudia wachezaji hao wakiwa katika hali ngumu za maisha huku namna ya kujiendeleza kielimu ikiwa imefikia ukomo kwa maana ya uwezo wa kujilipia karo huku timu walizokuwa wakizichezea zikiwa zimewaacha na kosa jingine kubwa ambalo hulifanya ni kujisahau kuweka akiba wakiamini nyota yao itaendelea kung’ara milele.
Siyo kwamba wachezaji wote hawana elimu lakini ni wengi wao ambao wana kiwango cha chini cha elimu na wamekuwa wakipata nafasi ya kucheza mpira kutokana na vipaji vyao lakini baada ya kiwango kushuka hujikuta wakitaabika na kuwa ombaomba wakiwa wametelekezwa na klabu zao.
Kwa mtazamo wangu ni wakati wa wachezaji wa Tanzania iwe wametoka katika shule za michezo au hawakupitia huko kucheza soka huku wakijipambanua na elimu ili kukabiliana na mizengwe ya soka ya Tanzania ambapo wachezaji kuachwa ni suala la kulala na kuamka.
Wachezaji hao hawapaswi kujisahau na kujikita katika soka zaidi badala yake watambue bado wanatakiwa kujipa nafasi ya kusoma ikiwezekana pale wanaposaini mikataba yao na klabu husika kuweka kipengele cha kupata fursa ya kusoma ili kujitengenezea mazingira ya baadaye hata baada ya kustaafu soka.
Lakini hali hii haiwagusi wachezaji peke yake hata wasanii wa fani mbalimbali ikiwemo ya uigizaji ambayo imekuwa na mashiko kwa jamii katika miaka ya hivi karibuni kujisahau kwao na kulewa na ustaaa waliokwishaupata badala ya kusoma.
Nasema hivi kwa sababu kuna baadhi ya wasanii iwe wa muziki au filamu baada ya kupata majina kupitia kazi zao za sanaa wameamua kuikacha shule na kujikita katika usanii zaidi.
Lakini leo hii kuna hao walioitosa shule na kuona haina umuhimu wamepotea kabisa kwenye ulimwengu wa sanaa na kukosa vyote kwa wakati mmoja.
Ni muhimu kwa wasanii wetu kujifunza kutoka kwa wasanii wa ughaibuni na siyo kuishia kuiga mambo ya laana tu na kuacha vitu vya muhimu ambavyo wasanii wa majuu wanavifanya, hususan katika masuala ya elimu.
Nina uhakika kuna baadhi ya wasanii wa Kibongo wanakosa mikataba yenye fedha kutoka nchi za mbali kutokana na kutokuwa na elimu ya kutosha katika masuala ya sanaa.
Binafsi nimefurahishwa sana na hatua ya meneja wa TipTop connection Babu Tale kuamua kumpeleka Dogo Janja shule, kwa kumlipia gharama zote za shule na mahitaji mengine.
Ni mameneja wachache sana ambao huamua kuwapeleka wasanii wao shule, hii imekaa vizuri sana kwa upande wa babu Tale na ni funzo kwa mameneja wengine.
Dunia ya sasa lazima ikimbizane na watu wenye elimu ili kuweza kuyakabili mazingira ni aibu kwa wasanii kukacha shule.
Nasisitiza hili kwa sababu taifa limekuwa likikosa vitu muhimu kama tuzo au makombe kutoka kwa wasanii ambao wanakuwa wameshiriki mambo mbalimbali katika nchi za wenzetu.
Kinachowafanya wasanii kushindwa kumudu ushindani ni kukosa elimu ya ile sanaa na wapo pia ambao hushindwa kutokana na lugha mbovu ya Kiingereza.
Kikubwa kinachowafanya wasanii kukacha elimu ni kulewa sifa ambazo ni za musimu tu, lakini wapo pia ambao wanastahili kupongezwa kutokana na juhudi zao za kujiendeleza kielimu iwe ni kwenye sanaa au mambo mengine.
Nasema hivi kwa sababu kuna wasanii kama Mr. Blue ambao walipopata majina makubwa wakalewa sifa na kuona shule haina umuhimu, ona sasa wako wapi? Wakiulizwa utasikia bado najipanga ndio majibu yao.
Najua kwa sasa atakuwa anajutia uamuzi wake wa kuitosa shule, kwani kwenye muziki havumi tena kwa sasa angekuwa na taaluma nyingine si angeitumia kujipatia kipato na kumrudishia heshima?
Tuache wivu na chuki, kiukweli Ally Kiba anastahili pongezi kwa kuipeperusha bendera ya Tanzania vyema kimataifa kutokana na wimbo wa ‘Hands Across the World’ uliotungwa na Robert Kelly au R Kelly.
Katika hili wasanii wanapaswa kujifunza na kuchukua hatua, najua wapo wenye viroho vya wivu lakini kimsingi wanatakiwa kuwa na wivu wa maendeleo na si vinginevyo.
Kwa mtazamo wangu nawaomba wachezaji na wasanii waweze kujiendeleza kielimu kwani inawanyima fursa ya kushiriki kwenye matamasha ya kimataifa na hivyo kujikosesha tuzo na heshima ambazo zingeweza kuitangaza Tanzania katika medani ya kimataifa

1 comment: